Mnamo Septemba 26, sherehe ya miaka 80 ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU) ilifanyika. Rais Xi Jinping aliwaandikia maprofesa wakongwe barua akipongeza BFSU kutimiza miaka 80, na kutoa salamu za dhati kwa walimu, wanafunzi na wafanyakazi wote.
Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu Bw. Zhong Denghua alisema kwamba tangu kuanzishwa kwa BFSU, imewatayarisha wanafunzi wengi wenye uwezo wa hali ya juu kwenye nyanja mbalimbali. Anatarajia kuwa BFSU itaendelea kuwatayarisha wanafunzi wenye uwezo mkubwa kwa kutekeleza kikamilifu kazi yake ya kimsingi.
Naibu Katibu Mkuu wa UM Bw. Movses Abelian alituma barua ya pongezi akipitia historia ya ushirikiano wa karibu kati ya Umoja wa Mataifa na BFSU, na alitumai BFSU itaendelea kuchangia kuwatayarisha wanafunzi hodari.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Prof. Wang Dinghua alitoa shukrani na heshima kwa watu wote walioiunga mkono BFSU. Alisisitiza kwamba mwaka 2021 ni mwanzo kwa safari mpya ya kuijenga China kwa pande zote kuwa nchi ya kisasa ya usoshalisti, BFSU itaendelea kuchangia pakubwa zaidi katika mchakato huo.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha BFSU Prof. Yang Dan alidhihirisha kwamba BFSU ni mwanzilishi, mtangulizi na mchangiaji katika elimu ya juu ya lugha za kigeni nchini China. Wanafunzi wa BFSU walikuwa wakiwepo kwenye harakati muhimu za kimataifa na walifanya juhudi kubwa kuzifanya China na ulimwengu zifahamiane zaidi. Alisisitiza kuwa watajifunga kibwebwe kuijenga BFSU kuwa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha kiwango cha juu zaidi duniani.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Peking (PKU) Prof. Hao Ping alitoa pongezi akisema kuwa miaka 80 ya maendeleo imeifanya BFSU kuwa chuo kikuu chenye sifa kubwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi.
Wageni wengi wanaoshughulikia mambo ya nje, diplomasia, biashara ya nje na lugha za kigeni walihudhuria hafla hiyo.