Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing kipo kwenye sehemu ya kaskazini ya Barabara ya Xisanhuan ambayo inagawanya chuo kizima katika kampasi ya mashariki na ya magharibi. Chuo chetu kinaongozwa na Wizara ya Elimu moja kwa moja na ni kimojawapo cha vyuo vikuu vilivyopewa kipaumbele katika miradi ya “211” na “985” ya kitaifa. Chuo chetu kinaongoza ufundishaji wa lugha za kigeni nchini China kwa historia yake ndefu, wingi wa lugha za kusomesha na ukamilifu wa mitalaa.
Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing kiliasisiwa mwaka 1941ambapo kilikuwa idara ya Kirusi ya chuo kikuu cha kijeshi mjini Yan’an. Baada ya kuasisiwa kwa China mpya, chuo chetu kilikuwa chini ya uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje hadi mwaka 1980. Mnamo mwaka 1994, chuo kilipandishwa hadhi kikawa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing.
Hivi sasa chuo kikuu kinasomesha lugha 101 za kigeni ambazo zimejumuisha lugha zote rasmi za nchi zenye uhusiano wa kibalozi na China zikiwemo lugha za Ulaya, Asia na Afrika. Zaidi ya hayo, chuo chetu kinasomesha lugha nafasihi ya Kichina, uandishi na upashanaji wahabari, siasa, sheria, uchumi na biashara, menejimenti, elimu na mengineyo.
Hivi sasa wapo wanafunzi wa shahada ya kwanza 5,700, wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu 3,900 na wanafunzi wageni 1,300. Chuo hiki kina walimu na wafanyakazi zaidi ya 1,300 pamoja na wataalamu 200 kutoka nchi 65 za dunia. Zaidi ya 90% ya walimu waliwahi kusoma ng’amboni.
Chuo Kikuu kimeanzisha ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi 299 za nchi na kanda 84. Pia kinaendesha taasisi 23 za Confucius zilizopo katika mabara ya Asia, Ulaya na Amerika.
Maktaba ya chuo hiki inahifadhi vitabu takriban mil. 1.57 na vitabu pepe mil.2.16, magazeti aina ya 1,081 na database 107. Pia chuo hiki kimejenga maabara ya lugha na akili bandia, makumbusho ya lugha za dunia na makumbusho ya historia ya chuo.
Chuo chetu kilikuwa kikienda sambamba na maendeleo ya taifa katika miaka 80 iliyopita na kimeandaa wahitimu mahiri wapatao elfu100 wanaofanya kazi katika sekta za diplomasia, tafsiri, uchumi, biashara, vyombo vya habari, sheria, fedha n.k. Kwa mfano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, inakadiriwa kuwa wapatao mabalozi 400 na waambata 2,000 na ushei walihitimu kutoka chuo chetu, ndiyo maana chuo chetu kimesifika kama ni “Mlezi wa Wanadiplomasia wa Jamhuri”.