Tarehe 7, Julai, Ubalozi wa Tanzania nchini China umefanya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kwenye mtandao. Walimu na wanafunzi wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU) wamealikwa kuungana nao katika maadhimisho hayo.
Mkurugenzi wa Idara ya Kiswahili ya BFSU Bw. Zhao Lei ametoa hotuba inayopitia historia na maendeleo ya kozi ya Kiswahili tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961. Profesa Feng Yupei ameipongeza UNESCO kufikia uamuzi wa kuweka siku maalum ya Kiswahili duniani pamoja na ubalozi wa Tanzania kuamua kuandaa maadhimisho hayo makubwa. Wanafunzi wa BFSU wameghani shairi maarufu la Shaaban Robert - “Kiswahili” kwenye maadhimisho ili kuonyesha furaha yao kwa sikukuu hiyo ya Waswahili wote ulimwenguni.
Balozi wa Tanzania nchini China Bw. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Omani Bw. Nasser Busaid, Kaimu Balozi wa Kenya Bw. Edward Kimani, Mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI Bi. Han Mei, mtaalamu wa sanaa za Kiafrika na mhitimu wa chuo chetu Bi. Han Rong, walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu vinavyosomesha Kiswahili nchini China na wadau mbalimbali wamejumuika katika maadhimisho hayo na kuisherehekea Siku ya Kiswahili Duniani kwa shangwe.