CHUO KIKUU CHA LUGHA

ZA KIGENI, BEIJING

Taasisi ya Sinolojia ya Kimataifa

发布时间:2019-04-28

Taasisi ya Sinolojia ya Kimataifa ilikuwa kituo cha utafiti kilichoanzishwa mwaka 1996 na imepandishwa hadhi tangu mwaka 2015. Taasisi hii inachunguza utafiti wa sinolojia ulimwenguni huku ikilenga kukuza na kueneza utamaduni wa kichina na mitalaa inayohusiana nao. Pia, inajihusisha na shughuli zifuatazo: kuchunguza historia na njia za uenezi wa utamaduni wa kichina duniani; kuchunguza matini, nadharia na mbinu za tafsiri za vitabu vya kale vya China; kuchunguza maendeleo ya mtalaa wa sinolojia katika nchi za nje; kutathmini taathira za utamaduni wa kichina duniani na mitazamo ya nje kuhusu China ili kudhihirisha umuhimu wa utamaduni wa kichina katika mawasiliano ya kiutandawazi.

Taasisi hii ina Kituo cha Utafiti wa Sinolojia ya Kimataifa, Taasisi ya Utamaduni wa Kichina na Kituo cha Tathmini ya Uenezi wa Utamaduni wa Kichina Duniani. Aidha, taasisi hii inachapisha majarida kadhaa ya kitaaluma kama vileSinolojia ya Kimataifa, Fasihi Linganishi na Mwingiliano wa Tamaduni, Taarifa za Utafiti wa Confucius DunianinaHistoria ya Elimu ya Kichina kwa Wageni.Licha ya hayo, taasisi hiyo ilianzisha Shirikisho la Kimataifa la Mtalaa wa Sinolojia, Shirikisho la Kimataifa la Elimu ya Kichina na Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Kimataifa la Confucius.

Pamoja na programu za shahada za Uzamili na Uzamivu katika fani ya Fasihi Linganishi na Mwingiliano wa Tamaduni, tunawakaribisha wanafunzi wageni kujiunga na programu ya M.A. katika Utafiti wa Utamaduni wa Kichina na Sinolojia ya Kimataifa ambayo kozi zote zinafundishwa kwa Kichina na Kiingereza.

Katika miongo miwili iliyopita, taasisi hii imekamilisha zaidi ya miradi 40 ya utafiti na kuchapisha vitabu 76, kazi za tafsiri 29, kamusi 2, vitabu 3 vya kiada na zaidi ya makala 100. Kwa miaka mitatu mfulilizo taasisi hii imetunukiwa tuzo la kwanza la chuo kutokana na mafanikio makubwa ya utafiti.

Taasisi hii imejenga ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi 33 kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Italia, Vatikani, Uswisi, Urusi, India, Japani, Jamhuri ya Korea, Singapore, Thailand, Malaysia na sehemu za Hongkong, Macao na Taiwan. Isitoshe, taasisi hii imetembelewa na wasomi wa nje zaidi ya 100 na imeandaa mihadhara zaidi ya 100 na makongamano ya kimataifa ipatayo 70.

No. 2 North Xisanhuan Road, Beijing, P.R.China. (100089)

OFFICE FOR INTERNATIONAL EXCHANGE AND COOPERATION

OFFICE OF CONFUCIUS INSTITUTES

OFFICE FOR OVERSEAS STUDENTS AFFAIRS

GENERAL ADMINISTRATION OFFICE

Copyright@BFSU.Support by ITC